Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, matembezi hayo yalifanyika jana, tarehe 28 Juni 2026 (7 Tir 1405), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Ashura 1448 Hijria. Mamia ya waumini wa Ahlul-Bayt (as), pamoja na viongozi mbalimbali wa kidini na wanajamii, walishiriki katika matembezi hayo yaliyolenga kuhuisha kumbukumbu ya msiba wa Karbala na kuenzi kujitolea kwa Imam Hussein (as) katika kutetea haki na uadilifu.
Washiriki wa matembezi hayo walitembea kwa utulivu huku wakionesha huzuni na maombolezo yao kwa mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), ambaye aliuawa kishahidi katika ardhi ya Karbala kwa kusimama dhidi ya dhulma, kulinda heshima ya Uislamu na kutetea utu wa mwanadamu.
Katika maadhimisho hayo, Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuhuisha ujumbe wa Ashura, akieleza kuwa mapambano ya Imam Hussein (as) yanabeba mafunzo ya kudumu kuhusu haki, ujasiri, umoja, mshikamano na kujitolea kwa ajili ya maslahi ya jamii.
Matembezi hayo yalihitimishwa kwa dua na maombi ya kuombea amani, umoja na mshikamano nchini Tanzania na duniani kote, huku waumini wakiahidi kuendelea kuenzi na kuendeleza ujumbe wa Imam Hussein (as) kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
![]() |
![]() |
![]() |
![]() |
![]() |
![]() |






Maoni yako